WALEMAVU 234 WAPATIWA MAFUNZO YA UKIMWI KAHAMA





JUMLA Walemavu 234 kati ya 900 waliopo wilayani Kahama wamepatiwa mafunzo ya kujikinga na maambuzi mapya ya Virusi Vya Ukimwi yaliyokuwa yakiratibiwa na Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania wilayani humo (SHIVYAWATA).

Mwenyekiti wa Shirikisho hilo wilayani Kahama Bw. Marko Nkanjiwa amesema mafunzo hayo yawajumuisha walemavu wote wakiwemo wasioona,Albino,wasiosikia,wa viungo na wenye mtindio wa ubongo, na kuwa mafunzo hayo yametolewa kwa kipindi cha miezi sita mfululizo.


Ameyasema hayo katika Kikao cha Tathimini ya mafunzo hayo ambapo amesema yameweza kuwajengea uelewa wa kujikinga na maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi kwa kudhaminiwa na Rapid Fund Envelope na kuwa yamesaidia pia kutoa uelewa kwa jamii kuachana na tabia ya kuamini kwamba Walemavu hawana maambukizi ya magonjwa ya zinaa hali inayopelekea kuwaingilia bila kuwepo kwa kinga.

Nae Muuguzi Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Kahama Bi. Emareciana Machibya amesema imani ya jamii nyingi kwamba Walemavu hawana matamanio ni potofu kwani hata wenye mtindio wa ubongo baadhi yao wanamatamanio ya kufanya ngono.

Amesema wanaoamini kwamba hawana maambukizi wanaipotosha jamii kwani tendo la ngono halichagui mtu hivyo mafunzo hayo kwa walemavu yana mantiki kubwa kwa kuwa hata wao wanatakiwa wajikinge na maambukizi ya Ukimwi na kuutaka uongozi wa Shirikisho hilo kuweka mipango ya kuwafikia walemavu wengine vijijini ili kutoa elimu hiyo kwa wote.

MWISHO. 

0 comments: