WAZAZI KAHAMA CHANZO CHA MIMBA ZA UTOTONI.
IMEDAIWA
kuwa baadhi ya wazazi wilayani Kahama huchangia ongezeko kubwa la watoto wao
kukatisha masomo kwa mimba huku wakiwa na umri mdogo hali ambayo inahatarisha maisha yao.
Hayo
yameelezwa na baadhi ya wasichana waliokatishwa masomo kwa kupata mimba wakiwa
na umri wa kati ya miaka 14 hadi 19 waliokuwa wakisoma katika shule za msingi
na sekondari kwenye kikao cha pamoja kati ya wazazi na watoto katika kijiji cha
Nyashimbi Kata ya Mhongolo wilayani Kahama.
Katika
kikao hicho kilichoratibiwa na Shirika la Kiota Women Health Development (KIWOHEDE),imedaiwa
kuwa hali ngumu ya maisha ya wazazi walioko vijijni ndio chanzo cha watoto wao
kujiingiza kwenye ngono wakiwa na umri mdogo.
Imebainishwa
kuwa baadhi ya wazazi hupokea zawadi ndogo ndogo kutoka kwa watoto wao wa kike
ikiwemo sukari,sabuni na nyama bila kuwauliza walikozitoa vitu ambayo mwisho wa
siku hujikuta wakiingiza kwenye ngono isiyo salama wakiwa wadogo na hivyo
kuambukizwa magonjwa ya zinaa ikiwemo Ukimwi na mimba za utotoni.
Ili
kuondokana na hali hiyo Afisa Mtendaji wa Kata hiyo Bw. Emanuel Kalolo amewataka
wazazi kuhoji watoto wao wanakozitoa zawadi hizo kuliko kusubiri kuhoji walikotoa
mimba hali ambayo haitasaidia kwakuwa tayari watakuwa wameisha chelewa na kuwa jukumu
la kuwatunza watoto hao ni la pamoja na si kuwatupia lawama walimu wa shule
wanakosoma.
Naye
Afisa Mradi wa Shirika la KIWOHEDE Bi. Bella Edward amesema katika kipindi cha
miezi mitatu iliyopita katika mradi wa uzazi wa mpango unaotekelezwa kwenye
Kata nne za Mhongolo,Busoka, Shilela na Lunguya imebainika kuwa idadi kubwa ya
wasichana kati ya miaka Kumi na Kumi na Tisa wako majumbani kwa kukatishwa
masomo na wazazi wao.
MWISHO.
0 comments: